Ngara na mazao ya kimkakati, Tiba sahihi ya kuondokana na umaskini kufikia 2030

By Titho Philemon Oct 25, 2024

Wilaya ya Ngara ikiwa ni moja kati ya wilaya zinazounda Mkoa wa Kagera yenye jumla ya Wakazi 383,092 ni wilaya ambayo imekuwa haina zao la kuaminika la kibiashara na badala yake yale mazao ya chakula kama Mahindi, Maharage, Njegere na mengineyo ndo yamekuwa yakitumika kwa vyote yaani CHAKULA na BIASHARA.

Hata hivyo hayo mazao ya CHAKULA – Biashara (Food & Cash Crops at once) yamekuwa hayawapatii tija wakulima chanzo ikiwa ni mfumuko wa bei (Price Fluctuation) kwenye masoko ambapo unakuta bei zinapanda na kushuka kihorela na hivyo kumuumiza mkulima wa kipato cha chini.

Kwa siku za hivi karibuni Mbunge wa Jimbo la Ngara amekuwa akisema kuwa amewasiliana na Wakala wa Hifadhi ya Chakula wa Taifa (National Food Reserve Agency – NFRA) kuhusu kuratibu na kusimamia ununuzi wa mazao ya Wakulima wa Ngara kama Mahindi mara tu msimu wa mavuno utakapoanza. ENDAPO ombi hilo kwa NFRA litafanyiwa kazi ndani ya Jimbo la Ngara itafaa sana na itatakiwa usimamizi uwe imara katika kuratibu vituo vya mazao (NFRA Wards Units – NWU) ili kama ni Wards Units (kwa maana ya kata) au Divisions Units (kwa maana ya kituo kwa kila Tarafa) basi ijulikane mapema ili wananchi na wakulima wasije wakapigwa changa la macho kama ilivyotokea kwenye masuala ya TEGESHA kwenye mradi wa TEMBO NICKEL yaani (Third Party Enjoyments versus Project Beneficiary Regret).

Katika hili la NFRA pamoja na usimamizi wa Mauzo Horela ili tuweze kuufikia uchumi imara kwa Ngara na wanaNgara kufikia 2030 viongozi, mamlaka na watawala wa Halmashauri ya Ngara wanapaswa kudhibiti na kusimamia ufuatiliaji wa masuala yafuatayo:-

  1. Kukemea na Kuzuia Uuzaji wa Mazao ya Chakula yakiwa shambani.

Halmashauri ya Wilaya ya Ngara katika kuhakikisha wanaNgara wananufaika na kilimo wanachokifanya bila kuathiri mstakabari wa maisha yao binafsi, Mwaka 2014 waliamua kutunga Sheria Ndogo (By-Laws) ambazo zililenga kuwa sehemu ya mwongozo kwa wananchi na wakulima wa Halmashauri ya Ngara.

Kwa mujibu wa Sheria Ndogo za (Kilimo na Hifadhi ya Chakula) za Halmashauri ya Ngara, 2014 chini ya Kifungu cha 12(f,g) ni kosa kuuza mazao bila kuweka akiba ya Mwaka mzima au zaidi lakini vilevile ni kosa kuuza mazao yakiwa shambani.

Halmashauri ya Ngara imekuwa haisimamii Sheria Hizi Ndogo (By-Laws) hali ambayo inachangia kudhoofisha ukuaji wa uchumi katika Halmashauri yetu. Kwasasa maeneo mengi ndani ya wilaya ya Ngara (Karibia 75% ya wilaya nzima) wananchi na wakulima wanauza mazao yakiwa shambani kitendo wanachokiita “KUGUZA URUSHUGWE”. Yaani Mkulima mwezi wa Disemba anauza Kilo Moja ya Maharage kwa Tsh 500/= yaani 1 Tone kwa Tsh 500,000/= (Laki Tano tu) na kuahidi kulipa baada ya mavuno.

Athari zake (URUSHUGWE) zimekuwa ni:-

  1. Kutelekeza Familia kwa baadhi ya Wanaume
  2. Kubakia katika mnyororo wa UMASKINI utokanao na udumavu wa kiuchumi
  3. Kuendelea kuwa stagnant (bumbuwazi) katika Fikra za kujikomboa kiuchumi.
  4. Kuvunjika kwa ndoa
  5. Kuongezeka kwa uhalifu.
    Ombi langu katika hili: SHERIA ILIYOPO ISIMAMIWE ILI KULINDA HALI YA MAZAO YA CHAKULA NA WAKULIMA WA NGARA.
  6. Kudhibiti Rushwa na Walanguzi kwenye masoko ya Kikata au Tarafa

Ili kuweza kutetea haki na unafuu wa Mkulima wa Ngara kwa haya mazao ya CHAKULA-BIASHARA uongozi, utawala na Mamlaka za Ngara kwa kuzingatia Sheria hiyo ndogo ya Halmashauri ya Kilimo na Hifadhi ya Chakula waweke utaratibu ili kuhakikisha kila mfanyabiashara wa nafaka au mazao ya kilimo katika masoko yetu awe amepata kibali maalumu kutoka kwa Afisa Biashara wa Halmashauri na katika kibali hicho mfanyabiashara huyo apewe bei elekezi kwa kila zao, baada ya hapo kila wiki Ofisi ya Biashara ya Halmashauri iwe inawasaidia wananchi wake kuhuisha (update) bei elekezi za bidhaa za Kilimo katika masoko kwa wiki husika au mwezi kwa utaratibu watakaoona unafaa. Hii itaisaidia kuwalinda wanajamii wa Ngara na wakulima dhidi ya wanunuzi wapigaji wasio na faida kwa Ngara yetu.

  1. Ziwepo Tozo maalumu za kibiashara (Additional Immi-Traders Charges) kwa Raia wa nchi jirani wanaokuja kununua mazao ya Chakula kwetu ziwekwe ili kudhibiti mfumuko wa bei na kuinua Pato la Halmashauri

Ikumbukwe kuwa Kwa Mujibu wa Sheria za Biashara nchini Burundi (majirani zetu kibiashara) ni Marufuku kwa Raia wa Burundi kuuza bidhaa nchini Tanzania au nje ya nchi, kwahiyo furaha ya mataifa ya jirani ni kuona sisi tukizalisha na kuwauzia wao kwa bei yao huku wao wakilenga faida (Win – Lose Situation) ndiyo maana msimu wa mavuno Baiskeli za Burundi na Magari vinapishana sana humu nchini kutafuta bidhaa.

Ili tuweze kufikia mafanikio makubwa kama wilaya na Halmashauri na kupata uwiano sahihi na bora kwa wananchi wetu kufikia Mwaka 2030 viongozi na watawala wanajukumu la kuhakikisha wanaratibu vizuri mizunguko hii ya walankuzi wa nje (Immi-Traders) na kuwaandalia Tozo maalumu na bei ya Ununuzi wa Mazao itakayokuwa imeratibiwa na Halmashauri yetu kwa uwazi na utaratibu maalumu. Hii itawafanya wananchi wawe na uchumi imara, amani na imani dhidi ya viongozi, watawala na Serikali yao na pia itaongeza Pato la Taifa (Rising-Up of the Nation’s GDPs)

Nasema hayo nikiwa natambua kuwa NFRA haitokuja kuhusika na mazao yote na badala yake kwa Mujibu wa kauli za Mheshimiwa Mbunge wa sasa wa Ngara Hon. RUHORO “NFRA watahusika na ununuzi wa zao la Mahindi tu”. Kwahiyo kwa hayo mazao mengine ambayo yatajumuisha Biashara Huria kutoka kwenye masoko yetu ya Ndani basi Ofisi ya Biashara ya Halmashauri ya Wilaya ya Ngara iingilie kati katika kuregulate bei kwa wanunuzi wazawa pamoja na kuimpose Additional Charges kwa wanunuzi wa nje (mataifa jirani) lengo ikiwa ni kujenga uchumi imara wa Halmashauri yetu ya Ngara, wanaNgara na Taifa letu kwa ujumla.

Mazao ya Kimkakati Ngara kama Tiba ya Kuondokana na Umaskini 2030

Nembo ya Halmashauri ya Wilaya ya Ngara imeainisha mazao makuu mawili ambayo ni Kahawa na Migomba (Ndizi) kama mazao ya kiuchumi ndani ya Halmashauri hii. Kwa miaka mingi sasa nembo hii imekuwa haina uhalsia kwasababu nusu ya wanaNgara (Zaidi ya 50%) wamekuwa hawayatumii mazao haya kama sehemu ya biashara walau Ndizi kidogo ambayo kila kaya ina uwezekano wa kuwa na Ndizi katika uwiano wa 1:23 wilaya nzima.

Kwasasa ninapenda kuipongeza serikali kupitia Bodi ya Kahawa nchini kwa kuona ni muda mwafaka sasa kwa wananchi wake kupata uwezeshwaji katika kilimo hiki ikiwa ni pamoja na kuwapatia mbegu bure kutoka katika vitalu mbalimbali vilivyoandaliwa.

Kwa Ngara tumebahatika kuwa na vitalu vitatu vyenye Miche ya Kahawa ambavyo kwa kiasi chake ENDAPO wananchi watakuwa wametilia maanani zoezi la uchukuaji wa Miche hiyo watakuwa katika nafasi nzuri za kujijenga kiuchumi katika siku za usoni. Kwakipekee niipongeze NGARA DC, Ofisi ya Mbunge wa Ngara (Hon. Ruhoro) pamoja na uongozi wa CCM wilaya ya Ngara kwa hamasa kubwa ambayo wamekuwa wakiitoa katika kuhamasisha wakulima kuchangamkia fursa hiyo. Ninaamini Tiba ya Umaskini kwa Ngara sasa inaenda kupatikana.

Hoja (Slogan) ya Mbunge wa Ngara Ndugu Ndaisaba George Ruhoro ya “Pesa kwa Wote ifikapo 2030” huenda ikakamilika ENDAPO usimamizi wa kisekta na kiutawala juu ya hayo niliyoyaeleza hapo juu utazingatiwa kwa umuhimu.

Kwa Mujibu wa Mheshimiwa Ruhoro, Kilo Moja ya Kahawa (Arabica) kwenye soko la kahawa ni Tsh 10,000/= na Kilo Moja ya Kahawa (Robusta) kwenye soko la Kahawa ni Tsh 6,000/= kwahiyo kama hivyo ndivyo, basi ni wazi na dhahiri kwamba Ngara na zao la Kahawa inaenda kufika mbali na kuwa Ngara inayong’ara ambayo imekuwa ikifikirika kwa kipindi kirefu katika Fikra zetu.

Kwa kuhitimisha: Ngara salama kiuchumi na kijamii itajengwa na wanaNgara wenyewe. Hii tabia ya sasa ya kutaka kuhusianisha Kila agenda dhidi ya mitazamo ya kisiasa hakika haitujengi kama WanaNgara.
Kwa pamoja tuunge mkono juhudi pamoja na yale mema yote yanayofanywa na viongozi pamoja na watawala wetu, na kwa pamoja TUKEMEE MAOVU YOTE yanayofanywa na viongozi pamoja na watawala wetu.
Kwa kufanya hivyo, tutakuwa watu sahihi, salama na MUHIMU katika ustawi na mstakabari mzima wa Maendeleo ya Wilaya yetu ya Ngara.

MUGIRE AMAHORO MEZA C’ANE!!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *