Msitumie Rungu Kuua Mbu, Wala Jiwe Kumtungua Kunguru

By admin May 12, 2025

Ameandika Baba Askofu Rev.Dr.Banson Bagonza (PhD), Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Karagwe
_______
Iliandikwa Tarehe 8/5/2025,

Papa wa 267 (Papa Leo XIV) amechaguliwa. Ni Mwana Chicago mwenzangu; Mwana CTU mwenzangu (CTU ni chuo kikuu cha Theolojia cha Kanisa Katoliki ambapo Bagonza kasoma hapo pia). Na ni Mwana Augustino mwenzangu (Msisahau Martin Luther alikuwa Padre wa O.S.A). Kwahiyo imekua siku njema kwangu.

Lakini pia imekua siku ngumu kwa sababu nimepokea taarifa kuwa “WASIOJULIKANA” watakuja kunimaliza. Hivyo nimeambiwa niishi kwa tahadhari. Sishangai maana ukimfuga mbwa ukamwachia aonje damu za watu, huwezi kumdhibiti tena na hawezi kuacha mwenyewe.

1. Kama kweli wanakuja; WAMEKOSEA. Wanaichafua serikali na taifa kwa jumla.

2. Kama hawaji, pia WAMEKOSEA. Bado Wanaichafua serikali na taifa kwa kuwaza kuja.

Kama wakija, nawaomba wasiharibu milango ya nyumba yangu na kuwafanya wanangu nitakaowaacha yatima waanze kufikiria kuitengeneza upya. Waniite nitatoka nijikabidhi.

Kama hawaji; namshauri mfuga mbwa awafungie mbwa wake ndani. Si kwa ajili yangu bali kwa ajili ya usalama wa mfunga mbwa mwenyewe na usalama wa kijiji chetu.

Huu ni mwaka wa uchaguzi. Hekima ni kutengeneza marafiki wapya kuliko maadui wapya. Usimuue mtu aliye tayari kufa. Hayo ni matumizi mabaya ya mauaji.

Awamu ya tano walikuja. Si lazima waje awamu ya sita hata kama awamu ya sita ni muendelezo wa awamu ya tano.

Iwe awamu ile au hii, hawa wasiojulikana ni waharibifu wa awamu zote mbili. Serikali makini (kama kweli haiwajui) ijitenge nao.

Wanaweza kufanya (kwangu) kwa sababu wameishafanya pasipotegemewa (TEC). Wakifanya wasijipongeze, wasipongezwe, na adhabu yao iwe ni kufanya MILELE.

Kama wakifanya; mwili utaoza, watu watalia, wengine watashangilia lakini watazaliwa wengine zaidi yangu.

Mungu analipenda taifa hili kuliko mimi ninavyolipenda. Hachelewi wala hawahi. Atasimama kulitetea.

Naishi katika jimbo la Waziri wa Mambo ya Ndani. Nina uhakika hajawatuma. Nawashauri wasitumie rungu kuua mbu aliyekaa kwenye kende za mfalme. Wala jiwe kumtungua kunguru aliyekaa kwenye kichwa cha Malkia.

Nawapenda Watanzania. Wakija kunichukua, tusipoonana tena, basi tutaonana kwa Baba kwa wale mlio na imani 

🙏🏽

By admin

Leave a Reply