Wakiongea na Ngaratv.com kwa nyakati tofauti wakazi wa Kijiji cha Murusagamba kata ya Murusagamba – Ngara, wamesema uhaba wa maji imekuwa kero hali inayopelekea mateso kwa wanawake kusafiri umbali mrefu kufuata maji mitoni. Halikadhalika wamesema wapo wananchi wengi ambao kwa uwezo wao wa kiuchumi wameanza kuchimba visima nyumbani kwao ili kujikimu na huduma hiyo baada ya kuonekana mradi wa serikali umeingiwa ukritimba kiasi cha kutokuwapa manufaa yoyote.
Aidha, Ngaratv.com ikiongea na baadhi ya wanawake wa Kijiji cha Murusagamba kwa masharti ya kutotajwa majina yao wanawake hao wamesema kuwa Ujio wa Waziri wa Maji Mheshimiwa Juma Aweso katika Kijiji hicho uliambatana na ingizo la kiasi cha Fedha Taslimu Shilingi Milioni Miambili na Hamsini (Tsh 250,000/=) kwa ajili ya kumaliza kero ya maji iliyokuwa ikiwakabili hapo awali. Wanawake hao wamedai kuwa maji yalipatikana kwa muda kidogo lakini hadi Muda huu hakuna DP hata moja ambayo inatoa maji ya uhakika ambapo DP mbili zinatoa maji kwa kusuasua na nyingine hazitoia maji kabisa. Aidha wameomba serikali ya Mama Samia na uongozi wa wilaya kuja kushughulikia kero hiyo ya maji kwa upesi maana bila maji ya uhakika maisha yao yatakuwa magumu na uchumi wao utazorota.
Baadhi ya Wanaume wa Kijiji cha Murusagamba kwa sharti la kutokutajwa majina yao wamesema hela ya mradi wa maji kutoka Serikali Kuu Tsh 250,000,000/= ilihujumiwa na viongozi wa kata kwa kile wanachodai kuwa hawaoni kilichofanywa na hela hiyo.
Katika kueleza wasiwasi wao wananchi hao wamesema Kitendo cha Diwani wa kata hiyo Mheshimiwa Sudi Mkubila kumteua Mdogo wake kwa jina la Abdul Mkubila kuwa msimamizi wa mradi huo kunawapa wasiwasi kwakuzingatia kuwa ni familia na mradi haujazaa matunda.
Aidha, wananchi hao wamesema Tank la kupokelea Maji linalotumiwa kupokelea na kusambaza maji siyo sehemu ya hela za mradi huo kutoka serikali kuu Bali lilijengwa na mfadhiri (aliyekuwa Padre wa Parokia ya Murusagamba) hali ambayo inawapa utata kuhusu matumizi ya hela ya mradi Tsh 250,000,000/= kutoka serikali kuu. Wananchi hao wameomba serikali, watawala, idara husika na TAKUKURU – NGARA kuingilia kati suala hili ili uchunguzi ufanyike na hujuma zibainike na wananchi waweze kuepukana na adha hiyo ya maji ambayo inawaathiri sana kijamii.