NGARA: WANANCHI WASISITIZA KUANZA HARAKA KWA MGODI ILI WAPATE AJIRA

By Na Mwandishi Apr 17, 2026

Na Mwandishi Wetu, Ngara.

Wananchi wa Kijiji cha Bugarama, Wilaya ya Ngara mkoani Kagera, wameiomba Serikali kuharakisha kuanza kwa mradi wa mgodi wa Tembo Nickel, wakieleza kuwa mradi huo ni tegemeo kubwa la maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika eneo hilo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi hao wamesema kwa muda mrefu mradi huo umekuwa ukipitia hatua za utafiti na maandalizi, hali iliyosababisha kusubiriwa kwa zaidi ya miaka 40.

Hata hivyo, wamebainisha kuwa katika miaka ya hivi karibuni kumeshuhudiwa hatua za maendeleo, ikiwemo ulipaji wa fidia kwa wakazi waliopisha maeneo yao kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Wananchi hao wameeleza kuwa kuanza rasmi kwa mradi huo kutachochea ongezeko la ajira kwa vijana, kukuza biashara ndogondogo, pamoja na kuongeza mzunguko wa fedha katika jamii.

Aidha, wameongeza kuwa shughuli za mradi huo zitasaidia kuboresha huduma za kijamii kutokana na ukuaji wa uchumi wa eneo hilo.

Pamoja na matumaini hayo, wameitaka Serikali na wawekezaji wa mradi huo kuhakikisha wakazi wa maeneo ya jirani wanapewa kipaumbele katika ajira na fursa nyingine zitakazotokana na uwekezaji huo, zikiwemo kazi za mgodini, usafirishaji na huduma mbalimbali.

Wamesema hatua hiyo itasaidia kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana na kuhakikisha jamii inanufaika moja kwa moja na rasilimali zilizopo.

Wananchi hao wameeleza kuwa wanaendelea kusubiri kwa hamu kuanza kwa mradi huo, wakiamini kuwa utakuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo katika Wilaya ya Ngara na Mkoa wa Kagera kwa ujumla.