WANANCHI WA KIJIJI CHA MAYENZI WATENGENEZA BARABARA KWA MAJEMBE

By Na Mwandishi Apr 24, 2026


Na Mwandishi Wetu, Ngara
Wananchi wa kijiji cha Mayenzi wilayani Ngara, mkoani Kagera, wamejitokeza kwa wingi kujitolea nguvu kazi katika ujenzi wa barabara inayounganisha kijiji hicho na Buhororo.
Hatua hiyo imefanyika Alhamisi, Aprili 23, 2026, ambapo wananchi hao walionekana wakifanya kazi kwa kutumia zana za jadi zikiwemo majembe na sululu, wakilenga kuboresha miundombinu ya usafiri katika eneo lao.
Barabara hiyo, licha ya kuwa ni njia ya mkato kati ya Mayenzi na Buhororo, imekuwa na changamoto kubwa ya kupitika kutokana na uwepo wa mawe makubwa yanayozuia usafiri kuwa rahisi kwa watumiaji mbalimbali.
Baadhi ya wananchi wamesema kuwa wameamua kuchukua hatua hiyo kutokana na umuhimu wa barabara hiyo katika kurahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii, huku wakiomba Serikali kuwasaidia kwa kuwapatia msaada wa kitaalamu na vifaa ili kuboresha barabara hiyo kwa kiwango bora zaidi.
Wameongeza kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutachochea maendeleo kwa kurahisisha mawasiliano na usafirishaji wa bidhaa kati ya vijiji vya Mayenzi na Buhororo.