WANANCHI WA NGARA WAIPONGEZA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA KWA PROGRAMU YA “SEMA NA WAZIRI”.

By Na Mwandishi May 7, 2026

Wananchi wa Wilaya ya Ngara wameipongeza Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuanzisha programu ya “Sema na Waziri” wakisema kuwa ni hatua muhimu katika kuimarisha utawala bora, uwazi na ushirikishwaji wa wananchi katika masuala ya maendeleo.
Wananchi hao wameeleza kuwa programu hiyo imefungua nafasi kwa wananchi kuwasilisha maoni yao, kuuliza maswali pamoja na kueleza changamoto zinazowakabili moja kwa moja kwa viongozi wa serikali. Wamesema hatua hiyo inaongeza uwajibikaji na kuimarisha uaminifu kati ya wananchi na serikali yao.
Kwa mujibu wa baadhi ya wananchi, programu hiyo ni mfano mzuri wa serikali inayosikiliza sauti za wananchi wake na inapaswa kuigwa na wizara nyingine pamoja na taasisi mbalimbali za umma.
“Tunawapongeza Wizara ya Katiba na Sheria kwa ubunifu huu. Programu hii inatoa nafasi kwa wananchi kusikilizwa na kupata majibu ya changamoto zao kwa uwazi zaidi,” amesema mmoja wa wananchi wa Ngara.
Baadhi ya wananchi akiwemo Joston Mkombozi, Irankunda Obeid na Nifasha Lazaro wamempongeza Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuanzisha programu hiyo wakisema imekuwa jukwaa muhimu la wananchi kusikilizwa na kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayowagusa.
Wananchi hao wameeleza matumaini yao kuwa programu hiyo itaendelea kuwa daraja la kuunganisha wananchi na viongozi huku ikisaidia kuharakisha maendeleo na utoaji bora wa huduma kwa jamii.

Pongezi zifike kwa Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria ni Dkt. Juma Zuberi Homera.