Ngara: Bodaboda wanahitaji hifadhi ya usalama wao kuliko Faraja za kisiasa.

By Titho Philemon Jul 31, 2024

Jamii inapaswa kutambua kuwa, HAKUNA maendeleo katika sekta yoyote bila siasa. Siasa hutengeneza viongozi viungo ambao wanaweza kubadili mtazamo wa kijamii kutoka kwenye hali duni na kuiendea nchi ya ahadi yenye maziwa na asali. Yote hayo yanaweza kufanikiwa tukiwa na viongozi wawazi, wakweli, wenye fikra sahihi, wanayapa kipaumbele maslahi ya umma na wenye kuzibeba shida za jamii kama za kwao.

Kikao cha Mbunge wa Jimbo la Ngara Ndugu NDAISABA GEORGE RUHORO pamoja na umoja wa Bodaboda wa Ngara (Maafisa Usafirishaji) cha July 29, 2024 kilikuwa cha kisiasa chenye mlengo wa maslahi binafsi kwa aliyewakutanisha (Mbunge) na siyo upendo wala lengo la kuwainua na kuwasaidia Bodaboda.

Najua wapo mtakaosema kwamba naona nongwa kwakuwa nyinyi ndio wanufaika wa mikakati hiyo. Hilo siwaingilii, niko radhi kuwekwa kwenye kundi la mtazamo wowote katika kutetea maslahi ya jamii yangu ya Ngara na Bodaboda wakiwemo.

Ninathibitishaje ubatili wa kikao cha Mbunge pamoja na Bodaboda wa Ngara ? Hoja ni mbili tu za Msingi.

  1. Hifadhi ya Usalama wa Maafisa Usafirishaji (Bodaboda): Hauwezi kusema unawasaidia Bodaboda kwa kuwachangia Milioni moja kuwajengea ofisi ya umoja wao ya wilaya wakati:- 86% ya Bodaboda hawana Leseni za kuendesha vyombo hivyo vya moto? Wakati 93% ya Bodaboda hawajalipia bima ya vyombo vyao vya moto ? Wakati 72% ya Bodaboda Ngara hawana elimu juu ya utumiaji?
  2. Sheria za Usalama Barabarani: Mheshimiwa Ruhoro angetakiwa kueleza mafanikio yake akiwa mwanasheria na mlezi wa Bodaboda wa Ngara KUFIKIA 2020 kabla Bodaboda hawajagombea Jimbo (kama alivyodai) na moja ya mafanikio iwe ni kuthubutu kutatua kero za Bodaboda KUFIKIA kiwango fulani ili suala la ujenzi wa Ofisi liwe ni suala la mwisho kukamilisha mshikamano na utulivu wa Bodaboda hao (Final Dot Point – FDP). Bodaboda wangepaswa wafundishwe Sheria za kuwalinda kwamba siyo kubeba kila mtu na kwamba kumbeba mtu chini ya Miaka 9 kwenye pikipiki ni kosa kisheria. Wakiwa na uelewa mpana wa Sheria za Usalama Barabarani watakuwa na kujiamini (confidence) na watakuwa na Uhuru zaidi katika biashara yao hiyo.

HAIINGII AKILI kuona tangu aingie kwenye ubunge ajali za Bodaboda zinaendelea na nyingi zikiwa zile zitokanazo na uzembe pamoja na elimu ndogo ya Usalama Barabarani halafu leo hii aseme yeye ni rafiki wa Bodaboda Ngara. Huo upendo unakuwa wa msingi upi na kwa faida ipi?

Angesema, ninaomba mnitafutie Bodaboda wote wa Ngara waliopoteza viungo vyao kwa ajali wapatiwe viungo bandia kama sehemu ya faraja – ningemuona wa maana na kuamini utu ndani yake katika kundi hilo.

Angejitoa kuwasaidia YATIMA, WAJANE na WAGANE ambao wategemezi wao wamepoteza maisha kutokana na Ajali za Bodaboda – ningeuhisi utu ndani yake na ningemuona anamaanisha anachokifanya.

Kusema wewe (Mbunge) ni daraja kati yako na Bodaboda Wakati:-

  1. Barabara ya Nyamagoma to Murusagamba via Murubanga haipitiki na unapokea hela ya Mfuko wa Jimbo ni kumaanisha nini ?
  2. Unakutana na Bodaboda wa Ngaramjini na kuwaacha Bodaboda wa Misenani na Mumilamila (vijijji vya interior) au wao siyo wapiga kura?
  3. Bodaboda hawajui hata Vehicle Inspection Report (VIR) ni nini ?
  4. Bodaboda na Traffic Police ni maadui kwa utofauti wa kwamba mmoja ni mjua Sheria mwenye mamlaka na mwingine ni Mvunja Sheria mwenye ujinga wa kuendesha kwa mazoea kwa kukosa elimu sahihi ?

Mwisho: Mheshimiwa Mbunge (Hon. Ruhoro), binafsi ninatambua kuwa wewe ni kijana mwenye umri wa kuipigania nchi hii. Endapo utaendelea kukoma na washauri haohao wenye ujuzi mdogo (Small Minded People) utajiundervalue na kuzidi kushuka grade kadri siku zinavyozidi kusonga.

Ukiona vijana wenye fikra Thabiti wamekukimbia kwa kuchoka kukupigania ujue Moja kwa moja chain yako nzima ya kiutendaji Ina dosari zisizovumilika.

Ngara itajengwa na Mbunge mwenye kuona kero ya Wanangara na kuitatua kwa maslahi mapana ya wanangara na siyo yule anayeona kundi gani linanjaa ili alishibishe kwa muda lipate nguvu za kumuimbia nyimbo za sifa na kuabudu pamoja na kughani mashairi na tungo za kusifia.

Wanangara tubadirike.
Bodaboda sanukeni!!📍
MUGIRAMAHORO NC’UTI ZANJE!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *