NGARA SASA NI SHWARI

By Na Mwandishi Apr 24, 2026


Na Mwandishi Wetu, Kabanga
Baadhi ya wananchi wa Mji wa Kabanga, wilayani Ngara mkoani Kagera, wameelezea kufurahishwa na hali ya utulivu wa kisiasa katika Jimbo la Ngara tangu alipoingia madarakani mbunge wa sasa, Dotto Jasson Bahemu.
Mbunge huyo aliingia madarakani kufuatia Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29 mwaka jana, na anaweka historia ya kuwa mmoja wa viongozi vijana waliofanikiwa kuliongoza jimbo hilo, akifuata nyayo za mtangulizi wake, Ndaisaba George Ruhoro.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi wamesema kuna tofauti ya mitazamo ya kiuongozi kati ya mbunge wa sasa na aliyemtangulia. Wamemtaja Bahemu kuwa kiongozi mtulivu na mwenye mikakati, tofauti na mtangulizi wake ambaye utendaji wake ulitafsiriwa na baadhi kuwa wa msisitizo mkubwa.
“Kijana ni mtu wa vitendo, hana papara, hata ukisikiliza hotuba zake zimetulia,” amesema Bw. Said, mkazi wa Kabanga.
Kwa upande wake, Mkidadi Minani amesema hali ya jimbo imeimarika zaidi kwa sasa, akibainisha kuwa kuna mshikamano mkubwa wa wananchi bila kujali tofauti zao.
“Jimbo limetulia kabisa. Ni tofauti na kipindi kilichopita. Kwa sasa kila mmoja anajiona ni sehemu ya uongozi,” amesema.
Naye Mama Salome ameongeza kuwa Jimbo la Ngara lina bahati ya kupata viongozi vijana wanaothubutu kugombea na kushinda, jambo linalochochea ushindani chanya wa kiuongozi.
Hata hivyo, wananchi hao wamekubaliana kuwa viongozi hao wawili wana uwezo, licha ya kutofautiana katika mitindo yao ya uongozi.