Wilaya ya Ngara haijawahi kuwa na mikutano ya koo kwa sababu za kisiasa, kiimani wala kwa itikadi ya aina yoyote. Tumekuwa tukishuhudia vikao vya koo mbalimbali kila mwaka na vingine kwa baada ya miaka miwili (kutokana na ratiba zao) malengo makuu yakiwa ni kutambuana, kupeana mikakati ya kulinda na kudumisha miiko, kuonyana na kufurahi pamoja kama ndugu wenye asili ya baba mmoja kihistoria.
Wilaya ya Ngara ikiwa ni moja kati ya wilaya nane (08) zinazounda mkoa wa Kagera inatambua uwepo wa koo mbalimbali kwa miaka mingi sasa. Tafsiri ya kijamii ya koo maana yake ni jumuiko la pamoja (kikundi) la watu wanaoshiriki mahusiano ya damu kutokana na misingi pamoja machimbuko ya familia zao. Kwa maana hiyo ukisikia neno “Ukoo” ujue wazi kwamba ni ndugu wa damu wanaotambuana na kutambuliwa kwa jina moja lenye maana ya pamoja kwao kama wanaukoo.
Kwa siku za hivi karibuni zimeibuka tabia za baadhi ya viongozi wanaotawala kwa sasa (viongozi wa kisiasa) kutaka kubaka taratibu za kimila kwenye koo mbalimbali lengo likiwa ni kujijengea ukubalifu wa kisiasa. Hali hii imekuwa ikiendelezwa na kuungwa mkono na makundi gushi ya kijamii pamoja na vijana wanaosadikika kununuliwa na wenye nia na mpango wa kujiimarisha kisiasa kupitia kivuli cha mila.
Tumeshuhudia mripuko wa makundi mawili ya wazee ndani ya Ngara ambapo kundi la kwanza linaonekana kushinikizwa na joto la kisiasa kutoa matamko ya kimila kwa niaba ya koo zao pasipokuwa na vibali vya wakuu wakoo zao. Kundi hili limewahi kuitwa kwenye ukumbi binafsi wa mwakilishi wa Jimbo la Ngara na kutoa matamko ya kushinikizwa, huku milo na posho ndogo ndogo zikithibitika kutolewa kwao kinyume na utaratibu pamoja na sheria za nchi hii.
Kundi la pili la wazee ni kundi la wazee halisi wa Ngara na wenye nyadhifa tofauti tofauti kwenye koo zao ambao wameonekana kwa nyakati tofauti tofauti wakitoa matamko ya kulaani kile kinachoendekezwa na wanasiasa kinachoashiria hofu na usalama wa mila na desturi za wanangara. Wazee hao katika tamko lao mbele ya waandishi wa habari walisikika wakisema kwamba walipatwa na shoti baada ya kupokea taarifa za kupatwa kwa mila zetu kama wanangara. Kauli za wazee wetu yaliashiria hali ya huzuni katika suala zima la mila pamoja na siasa za mpasuko zinazotaka kuzitumia mila za wanangara kama kivuli cha wao kuyaficha madhaifu yao huku suala la KUUTAKA UCHIFU likiacha msisimuko na butwaa ya ajabu yake kwa wazee wetu.
USHAURI WANGU KWA WANASIASA WA NGARA:-
01. Lindeni heshima ya mila za wale mnaowaongoza kwakuwa mila zao ndo fahari yao na ndio chachu pekee ya amani ambayo inawafanya watawalike. Kuwagawa kwa misingi ya koo zao ni kutaka kuwapandikiza chuki ya muda mrefu hususani kwa koo zile zitakazoonekana zikipendwa zaidi na mtawala kuliko nyingine.
02. Viongozi mkiendekeza koo kwenye tawala za kisiasa na kiserikali wanangara tutashindwa kusaidiana kupeana fursa mbalimbali kwa misingi ya kwamba fulani siyo mtu wa ukoo wangu wakati wote hapo ni wanangara tena wenye asili moja ya kiutamaduni. Viongozi chunga sana msituelekeze kibra. Tuhurumieni sana msitufanye mbuzi wa kuomboleza kwenye sikukuu zenu, tutapoteana kwakweli.
03. Kiongozi kuamsha suala la koo kwenye tawala za sasa ni kudharau sheria za nchi yetu na kiapo cha uadilifu katika uongozi na utumishi wao. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 chini ya ibara ya 12 na 13 inatambua kuwa binadamu wote tuko sawa na tuna haki sawa mbele ya sheria, sasa ninashangaa huo mpango wa koo unalenga kutujengea nini hasa (viongozi waza sana, msitupoteze).
Kwa kuhitimisha!
Hakuna koo bila familia, hakuna taifa bila familia, hakuna dunia bila familia na hakuna mafanikio bila familia. Ngara ni Mali ya Wanangara kwahiyo familia zetu ambazo walezi wetu ndo wazee wetu zina mamlaka ya kubatilisha kila mpango mchafu (ovu) wenye nia ya kutusambaratisha na kutugawa Kama wanangara ambao tumedumu kwa upendo na umoja kwa muda mrefu. Chonde chonde, wanasiasa wa vyama vyote pigeni siasa ila kwenye koo zetu na mila zetu kwa ujumla HESHIMU SANA. Watu epukeni kutumika hovyo, kumbukeni kuwa kuna maisha tena Ngara baada ya siasa, tusilisahau hilo.