Viongozi Na Watumishi Ngara Jiimarisheni Kukabiliana na Joto la Kisiasa Kuelekea Chaguzi Zijazo 2024/2025

By admin May 16, 2024

Na:- 

*Titho D. Philemon*

*KWAKUANZA, ninatambua kuwa “Uchaguzi”* ni utaratibu wa kawaida wa demokrasia wa kuwapata wawakilishi wa kisiasa ambao umekuwa ukitumika tangu karne ya 17 hadi sasa.

Uchaguzi huwapa wananchi fursa ya kutoa mamlaka yao kwa kundi dogo la watu ili waweze kuunda serikali. Ibara ya 8 (1) (a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 inatamka kwamba, Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii na kwa hiyo wananchi ndio msingi wa mamlaka yote na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba hii. *Kutokana na Ibara hii ya Katiba yetu* ni dhahiri kwamba wananchi ndio maboss wa serikali yoyote inayokuwa madarakani kwa wakati huo bila kujali itikadi za aina yoyote ile zilizoko miongoni mwa Raia.

*Ndani ya wilaya yetu ya Ngara kwasasa* kumekuwa na vuta nikuvute ambayo kwa upande mmoja inaonyesha *ukomavu wa kisiasa* na kwa upande mwingine inaonyesha wazi *ushamba wa kisiasa*. Hii inatokana na hali halisi ya ushindani inayoonekana kwasasa.

*KWANINI UKOMAVU WA KISIASA NGARA ?*

Ni mwaka 2024 pekee tangu nikue na kuijua historia ya kisiasa kwa Ngara ambapo nimeshuhudia msuguano mkali wa kiitikadi hata kabla ya muda kufika huku *uongozi uliko madarakani* nikimaanisha wabunge na madiwani wakizidi kujihami kwenye nyadhifa zao kwa jasho na mifadhaiko mingi ilimradi wapate ukubarifu wa raia kwenye masanduku ya kura wakati utakapofika. 

Pressure pamoja na fukuto la kisiasa linaloendelea hivi sasa limeiingiza Ngara katika majaribio tofauti tofauti (flexible trials) kwa baadhi ya viongozi kujaribu kuunda mbinu butu ambazo kimsingi zimekuwa zikigonga mwamba baada ya kuwa zimekosa uungwaji mkono wa watu pamoja na makundi mbalimbali ya kimila na kijamii. *Itoshe kusema kuwa* NGARA imekomaa kisiasa.

*KWANINI USHAMBA WA KISIASA NGARA ?*

Ushamba unakuja baada ya ongezeko la joto kuelekea katika chaguzi zijazo 2024/2025 *ambapo* yameingia makundi ya vijana ambao kwa namna wanavyoendesha siasa zao ninawaita washamba wa siasa. Tuna vijana wa vyama vya upinzani na Mimi nikiwemo ambao moja ya majukumu yetu makuu imekuwa ni kuibua changamoto za kiutendaji za viongozi walioko madarakani ili kuwapa nafasi ya kuweza kujisahihisha kwa maslahi mapana ya jamii yetu ya Ngara. 

*Ninawasihi sana* viongozi na watumishi wetu wa serikali wa wilaya ya Ngara kuongeza umakini, busara, maarifa, hekima na utambuzi wa ziada katika utendajikazi wao wa kila siku katika ofisi zao ili waweze kukabiliana vilivyo na joto hili la kisiasa.

Viongozi na watumishi wa halmashauri yetu ya Ngara ninaomba kuwashauri yafuatayo:-

1. Waonye na kukemea udaku pamoja na taarifa zenye kuzua taharuki katika jamii zitakazojaribu kutolewa na wanasiasa *pasipo uthibitisho.*

2. Tuhuma zitakazotolewa na upande wa kwanza wa siasa kuelekea upande wa pili *ziwe na uthibitisho anuai* ili kuepusha hali za kuchafuana.

3. *Mahakama ziwe huru kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria pale itakapobidi* ikiwa ni pamoja na kuadhibu kwa haki vitendo vyote vyenye nia ovu ambavyo kimsingi vinaweza kuhatarisha usalama wa raia katika kipindi hiki tunapoelekea uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 na uchaguzi mkuu 2025. 

4. Wanasiasa wahamasishwe na wafunzwe kujenga hoja kwa akili pamoja na uthibitisho/ vielelezo halisia pale wanapotaka kushambuliana kisiasa.

5. Jeshi la Polisi wilaya ya NGARA lisimamie haki, Sheria pamoja na mienendo mizima ya Jinai ili kuhakikisha kosa linapofika pale linashughulikiwa kwa ueledi na siyo kwakuwa washtakiwa ni chama tawala mnapiga mkwala kwamba jalada mara liko ofisi ya wakili wa serikali kuweni wavumilivu hali za namna hiyo zitalivunjia heshima jeshi la Polisi.

6. Mkuu wa wilaya kwa kushirikiana na ofisi ya TAKUKURU (W) NGARA ninawaomba kwa upekee kabisa waweze kukabiliana na vitendo vya Rushwa vinavyoendelezwa na baadhi ya viongozi waliopo madarakani katika namna na style tofauti.

*Nikiwa ninatambua kuwa* siasa ni kunadi sera za vyama vyetu pamoja na vipaumbele vyetu sambamba na mafanikio tuliyofikia hadi sasa (kwa viongozi walioko madarakani), basi tufanye hivyo *bila kupotosha umma!*

*TUSICHAFUANE!* 

CCM ndicho chama kinachounda serikali iliyopo madarakani kwasasa, lakini kuwa CCM haiwezi kuwa TIKETI ya kuvunja sheria na kuanza kuwachafua *watu wa ndani ya vyama vyetu* na wale *wa nje ya vyama vyetu* HUO NI USHABA WA KISIASA.

Viongozi na watumishi wetu wa Ngara ninawaombea hekima, busara, ueledi na upendo katika kutekeleza majukumu yenu katika kipindi hiki cha joto la kisiasa.

Mungu ibariki Ngara!

Mungu ibariki Tanzania!

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *