Ni takribani mwezi mmoja sasa toka kupanda kwa joto la kisiasa katika jimbo la Ngara linalopatikana kaskazini Magharibi mwa Tanzania mkoani Kagera. Vuta nikuvute na taharuki za kisiasa na kijamii imekuwa ni sehemu ya joto hilo la kisiasa wilayani Ngara hali iliyopelekea kuibuka kwa mpasuko mkubwa wa kijamii huku jamii ikishuhudia uwepo wa kundi la Wasaka ubunge dhidi ya kundi la Wasakatonge.
Mnamo Mei 28, 2024 Mkuu wa Wilaya ya Ngara Col. Mathias Julius Kahabi kupitia kikao chake cha ulinzi na usalama wilaya kilichohusisha wazee maarufu, na viongozi wa dini wa wilaya hii, alitoa MATAMKO dhidi ya Mbunge wa Jimbo hili pamoja na jamii kujiepusha na masuala ya uchifu kwa maana kwamba masuala hayo yalishafutwa tangu mwaka 1965 na hadi sasa hayatambuliwi kwenye sheria za nchi yetu.
Hii inakuja ikiwa ni baada ya kutanda kwa taharuki ya kijamii mapema Mei 8, taharuki ambayo ilihusisha nia ya Mbunge wa Jimbo la Ngara Mh. Ndaisaba George Ruhoro kutaka kutawazwa kuwa chifu wa koo zote za Ngara.
Katika hali ya kushangaza, vijana wa Ngara pamoja na baadhi ya wazee wa wilaya hii wamejikuta wakiingia katika vita mbaya ya kisiasa huku makundi yanayomuunga mkono Mbunge wa sasa yakionekana kuwaka zaidi katika vita hii ya siasa dhidi ya watu wote wenye nia na ubunge wa wilaya hii wajulikanao kama WASAKA UBUNGE. Baadhi ya wafuasi wa Mbunge huyu wakiongozwa na na ndugu JOSIAS CHARLES ISSAYA wamekuwa wakiwaondoa kwenye makundi sogozi ya WhatsApp wale wote wanaojaribu kuwa kinyume na Mbunge wa Jimbo hili kitendo ambacho kimewafanya wanajamii wamuite CHAWA.
Akiongea na Ngaratv.com mmoja kati ya wananchi wa Kazingati, kata ya Keza wilayani humu (jina limehifadhiwa), amesema kuwa, kero za wahudumu wa afya katika maeneo hayo zimefanya jamii wakiwemo akina mama kukosa amani kutokana na michango holela isiyowekwa wazi inayoratibiwa na wahudumu hao. Baada ya kusambaa kwa sauti ya ndugu huyo kwenye makundi mbalimbali ya WhatsApp wachangiaji wamekuja na hisia tofauti dhidi ya Wasakatonge (wapiga kura) wa Ngara wanateseka na shida ndogo ndogo wilayani humo huku Mbunge wao akiwa bize kujenga maghorofa na kujiimarisha kisiasa kwaajili ya chaguzi zijazo.
Ngaratv.com imejaribu kumtafuta diwani wa eneo hilo lakini upatikanaji wake haukuzaa matunda.
Sauti ya mmoja wa wananchi wa Jimbo la Ngara akiomba msaada wa viongozi kero ya huduma za afya Kijiji cha Kazingati, kata ya Keza – Ngara